Zanzibar. Saa 24 zimebaki kabla ya
mshambuliaji, Emmanuel Okwi wa Yanga na beki Donald Mosoti wa Simba
kutangazwa kuwa si wachezaji wa klabu hizo.
Viongozi wa Simba na Yanga wanajua kuwa kesho ni
siku ya mwisho ya kufanya usajili hivyo wanatakiwa kufanya uamuzi sahihi
ni wachezaji gani wanataka kuendelea kuwa nao kati ya Mosoti au Butoyi
Hussen kwa Simba na Okwi au Hamis Kiiza kwa upande wa Yanga.
Yanga ina wachezaji sita wa kigeni kama ilivyo kwa
Simba, lakini kuachwa kwa Okwi na Mosoti kutategemea nguvu ya hoja kati
ya makocha na viongozi wa timu hizo kubwa nchini.
Mbrazili Marcio Maximo ameshaweka wazi kuwa
anawajua wachezaji watano wa kutoka nje katika kikosini chake bila ya
kumjumuisha Okwi.
Maximo alisema: “Ninao wachezaji watano tayari wa
kutoka nje ya nchi kwenye timu yangu, hao ndiyo nitakaofanya nao kazi
msimu huu.
“Huyo Okwi sijamuona na hadi leo hajaripoti kwenye
timu yangu nifanyeje? Nitafanya kazi na hao tu.” Maximo ana wachezaji
wa kigeni, Kiiza (Uganda), Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite
pamoja na Wabrazili Andrey Coutinho na Santos Santana ‘Jaja’.
Lakini, Yanga ina mkataba na Okwi hivyo kufanya
kuwa na wachezaji sita, idadi ambayo hadi kesho siku ya kufunga dirisha
la usajili, itatakiwa kupunguza mmoja.
Wakati hali ikiwa hivyo Jangwani, viongozi wa
watani wao Simba, juzi walikutana Zanzibar ili kumaliza suala la
usajili wa beki wao mpya, Mrundi Butoyi na kumtema Mosoti.
Viongozi hao waliokutana ni Makamu wa Rais,
Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kassim
Dewji, Mjumbe na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collins Frisch,
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Mohammed Nassoro na Makamu wake, Idd
Kajuna pamoja na wajumbe, Adam Mgoyi, Mohamed Omary na Hussein Simba.
Dewji alisema wameangalia viwango vya wachezaji wao na kuridhika kuwa Butoyi amecheza kwa kiwango cha juu zaidi.
Kuhusu hatima yake alisema itajulikana ndani ya
siku mbili baada ya kukaa na kocha ili kuamua nani abaki kati ya Mosoti
na Butoyi, ingawa inasemekana pendekezo lao ni kumsajili Butoyi.
“Dirisha la usajili linafungwa Jumatano ni lazima
tufanye uamuzi kati ya siku hizi mbili, timu yetu ipo vizuri sasa hivi
na upungufu tulionao tutazungumza na kocha ili arekebishe mapema.
“Butoyi tumemwona, ni mchezaji mzuri na kikubwa hapa ilikuwa ni
kujiridhisha tu ila hatuwezi kufanya lolote mpaka tukutane na kocha
ambaye pia amemuona kwenye mazoezi,” alisema Dewji.
Lakini habari za ndani zinasema kikao hicho kilimalizika saa nane usiku bila kufikia uamuzi.
“Walitaka kufanya uamuzi wa kumpa mkataba Butoyi,
lakini kocha amewaambia wasubiri kwanza atawapa jibu kabla ya usajili
kufungwa.
“Wengi wanataka Butoyi asajili kwani kigezo
wanachotumia ni kwamba Mosoti umri umekwenda, kiwango chake kimeshuka na
alionyesha kutaka kuondoka hivyo wanataka wamwachie awe huru.”
Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema: “Ni lazima
nifanye uamuzi sahihi, leo (jana) jioni nitakuwa na jibu kuhusu nani
kati ya hao atabaki, ila Butoyi na Mosoti wote ni wazuri.”
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment