Home Traders

Home Traders

Tembelea TK FM Redio 88.5 Tanga

Wednesday, 3 September 2014

Majambazi wateka magari, wapora mali

Morogoro.Watu wanaodhaniwa kuwa majambazi walifunga Barabara ya Morogoro - Iringa katika eneo la Njia Panda ya Kilosa na baadaye kuteka magari na kupora mali za watu.
Tukio hilo lililotokea saa 8:30 usiku wa kuamkia jana, limekuja siku moja baada ya polisi mkoani hapa, kumtia mbaroni raia mmoja wa Burundi akiwa na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika utekaji wa magari.
Vifaa hivyo ni pamoja na darubini, mnyororo wenye misumari, visu 10, maturubai na mabomu ya milipuko.
Kwa mujibu wa baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, watekaji walikuwa wakirusha mawe na kuvunja vioo vya magari yaliyokuwa yamefika katika eneo hilo.
Mmoja wa mashuhuda hao ambaye ni dereva wa gazeti hili, Deo Ngangaa alisema walikuwa wakisafiri kutoka Iringa kuelekea Morogoro na walipofika jirani na eneo la tukio, walisikia milio ya risasi na mawe yaliyokuwa yakirushwa.
Alisema walilazimika kujificha hadi milipuko hiyo ilipomalizika ndipo wakaendelea na safari.
Hata hivyo, Dereva huyo alisema walipofika Njia Panda ya Kilosa, kando ya barabara waliona magogo na mawe huku magari matatu yakiwa yamepinduka.
Alisema walishuhudia watu kadhaa wakiwa wameanguka chini akiwamo dereva wa gari lililokuwa likipelekwa Zambia ambaye pia ni raia wa nchi hiyo aliyejeruhiwa kwa kupigwa pamoja na mjamzito. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.
Chanzo Mwananchi.

No comments:

Post a Comment