HATIMAYE sakata la kuchota fedha kwenye Akaunti Maalum ya Tegeta
Escrow, zilizohifadhiwa kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), litajadiliwa
bungeni Novemba 27 na 28 mwaka huu, imebainika.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana
juzi, ambapo pamoja na mambo mengine ilijadili na kutengua kitendawili
cha kashfa ya mradi wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Independent Power
Tanzania Ltd (IPTL), ijadiliwe bungeni.
Kikao hicho cha Kamati ya uongozi, kililazimika kujadili sakata hilo
kutokana na maagizo ya Naibu Spika, Job Ndugai, aliyoyatoa juzi wakati
akitoa mwongozo wa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kufulila
(NCCR-Mageuzi), kutaka Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili
sakata la IPTL.
Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho cha Kamati ya Uongozi, kiliipasha
Tanzania Daima kuwa, kamati hiyo imeagiza ripoti zote mbili, kuanzia ile
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhusu kashfa hiyo, zijadiliwe
bungeni.
Uamuzi huo, huenda ukawa mwiba kwa Serikali ambayo juzi kupitia kwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi, ilisema ripoti ya CAG na Takukuru hazijakamilika, hivyo suala
hilo halitajadiliwa kwenye mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea
mjini hapa.
Habari zinasema, wenyeviti wa Kamati zote zinazounda Kamati ya
Uongozi, walikubaliana na hoja ya Kafulila kutaka ripoti hizo zijadiliwe
katika Bunge hili.
“Kamati ya uongozi ilianza kikao chake majira ya saa 11 jioni na
kumaliza saa tatu usiku. Wenyeviti wa kamati wote, waliungana na hoja ya
Kafulila na ikaamuliwa ripoti hizo zijadiliwe Novemba 27 na 28,”
alisema mtoa habari wetu.
Habari zaidi, zinasema kuwa tarehe ya kujadili ripoti hizo zimewekwa
mwishoni ili kuogopa kuharibu ratiba ya Bunge endapo itatokea baadhi ya
viongozi kutakiwa kuwajibika.
Naibu Spika wa Bunge, Ndugai, alipoulizwa uamuzi wa Kamati ya
Uongozi, aliliambia gazeti hili kwamba, kamati hiyo imeamua ripoti hizo
zije bungeni katika muda waliopanga.
“Ukitaka kujua lini, angalia ratiba ya shughuli za Bunge hili utaiona,” alisema kwa kifupi Ndugai.
Wabunge wagawanyika
Kutokana na hatua hiyo, wabunge wa Bunge la Jamhuri wamegawanyika katika makundi mawili.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, umebaini kuwa kundi kubwa la
wabunge wanahamasishana, tena kupitia vipeperushi kutaka wahusika wa
kashfa hiyo wang’oke, huku kundi la pili ambalo ni la wabunge wachache,
likipanga mikakati kuwanusuru watuhumiwa.
Watuhumiwa katika kashfa hiyo waliotajwa bungeni na Kafulila ni
pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Katibu
Mkuu wake, Eliachim Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini
(Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba.
Sakata hilo liliibuka tena juzi siku ya kwanza bungeni, baada ya
Kafulila kuomba mwongozo wa Spika kutaka Bunge liahirishe shughuli zake
ili kupata fursa ya kujadili ripoti ya CAG na Takukuru za uchunguzi wa
kashfa hiyo.
Kabla ya Naibu Spika Ndugai kutoa mwongozo wake, Waziri Lukuvi alipinga mwongozo huo kwa madai kuwa ripoti hizo hazijakamilika.
Kauli ya Lukuvi, ilimuibua Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali
(NCCR-Mageuzi), ambaye aliibana Serikali ilete ripoti hizo bungeni,
vinginevyo Dodoma hapatakalika.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), akichangia hoja hiyo,
alilitaka Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza kashfa hiyo wakati
Serikali kupitia kwa CAG na Takukuru ikiendelea na uchunguzi wake.
Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika Ndugai, alisema kwa kuwa Kamati ya
Uongozi ya Bunge ilitarajiwa kukutana juzi jioni, ambapo pamoja na mambo
mengine itajadili hoja hiyo ya IPTL na kutolea ufumbuzi.
Tayari nchi wahisani zimetangaza kuikatia misaada Serikali ya zaidi ya sh trilioni 1 kutokana na kashfa hiyo.
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa kutokana na kutoelewana kuhusu
gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa
Tanesco.
Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID), katika uamuzi wake wa
Februari 2014, ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango
cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.
Kwa uamuzi huo, ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa
kwenye akaunti hiyo maalumu ya Escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na
Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali,
lakini badala yake fedha hizo zilitoweka ghafla kwenye akaunti hiyo.
No comments:
Post a Comment