KLABU
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jana ilitimiza miaka nane
tokea ipande rasmi Ligi Kuu mwaka 2008 tarehe kama ya jana (Julai 27),
ambapo ilipanda baada ya kuichapa Majimaji ya Songea mabao 2-0, mechi
iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Mabao ya Azam FC kwenye mchezo huo yote yalifungwa na John Bocco
‘Adebayor’ yote yakitokana mipira ya adhabu ndogo, ambapo ushindi huo
uliifanya Azam FC kuongoza kituo cha Dodoma kwa kumaliza ikiwa na jumla
ya pointi saba.
Pointi hizo saba zilipatikana baada ya Azam FC kuifunga Majimaji
(2-0), ikaichapa tena Kijiweni FC ya Mbeya (2-1) na sare bila ya
kufungana aliyoipata dhidi ya Mbagala Market ya Mbagala jijini Dar es
Salaam (hivi sasa African Lyon).
Kikosi cha Azam FC kilichocheza siku ya kupanda daraja kiliundwa na
kipa Idd Abubakar ambaye ni Kocha Msaidizi wa makipa wa Azam FC hivi
sasa, Malika Ndeule, Paulo Nyangwe ‘Mitindo’, Meneja wa timu hiyo hivi
sasa Luckson Kakolaki, Boniface Pawasa (C), Adam Ngido ‘Popa’, Salum
Abubakar ‘Sure Boy’, Steven Nyenge, John Bocco ‘Adebayor’, Kassim
Kilungo na James Adriano.
Mpaka sasa wachezaji walobakia ni wawili tu kutoka kwenye kikosi
hicho, nahodha Bocco na Sure Boy, ambao mpaka sasa wametimiza mwaka wa
nane wakiwa na Azam FC.
Wakati huo Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati ilikuwa
chini ya makocha Mohamed Seif ‘King’ na Msaidizi wake, Habib Kondo,
ambapo mechi hiyo ya mwisho ilishududiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa
zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni.
Ikiwa na miaka nane tu tokea ipande, Azam FC imefanikiwa kuleta
upinzani mkali kwa vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga, ambapo mwaka
huu iliweza kufuzu kwa mara ya tano mfululizo kushiriki michuano mikubwa
ya Ngazi ya Klabu Barani Afrika na hii ni mara baada ya kushika nafasi
mbili za juu kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), lakini kwa
mwaka huu ikifuzu kufuatia kuwa washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho
(Azam Sports Federation Cup).
Ndani ya miaka nane tu Ligi Kuu, Azam FC inayomilikiwa na familia ya
Mfanyabiashara Maarufu Afrika Mashariki na Kati, Alhaji Said Salim
Bakhresa, ambaye ni mmiliki wa Makampuni ya Bakhresa, imeweza kutwaa
mataji mawili makubwa, moja likiwa la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
(VPL) msimu wa 2013/14 ikitwaa kwa rekodi ya aina yake ya bila kufungwa
mchezo wowote.
Mechi ya mwisho iliyoipa ubingwa huo Azam FC ilikuwa ni dhidi ya
Mbeya City Aprili 13, 2014 walipoifunga mabao 2-1 ndani ya Uwanja wa
Sokoine, Mbeya yakifungwa na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba huku John
Bocco akiweka rekodi nyingine ukiacha ile ya kuipandisha daraja timu kwa
kutupia bao la ushindi likiwa la pili kwenye mchezo huo.
Taji lingine ni lile la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati
(CECAFA Kagame Cup) walilotwaa Agosti 2 mwaka jana kwa kuwachapa
mabingwa wa Kenya Gor Mahia mabao 2-1, Bocco alijiwekea rekodi nyingine
tena kwa kufunga bao la kwanza lililowapa nguvu ya kutwaa ubingwa huku
Kipre Tchetche akihitimisha kwa kufunga la pili kwa mpira wa moja kwa
moja wa adhabu ndogo.
Mbali na mataji hayo makubwa, pia Azam FC ambayo ina kituo cha kukuza
vipaji (Academy) kinachofanya vizuri kwa kutoa wachezaji bora nchini,
imefanikiwa kutwaa makombe mengine madogo, ubingwa wa Mapinduzi Cup mara
mbili (2012 na 2013), Kombe la Hisani lililofanyika mjini Kinshasa, DR
Congo (2012) pamoja na ubingwa wa Kombe Maalum la timu nne lililofanyika
jijini Ndola Zambia mwaka huu.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB pamoja na kinywaji safi cha
Azam Cola, ilitwaa taji hilo nchini Zambia mbele ya wenyeji Zesco United
na Zanaco pamoja na mabingwa wa Zimbabwe msimu uliopita Chicken Inn.
Mbali na makombe ya timu kubwa, Azam Academy nayo imeitangaza vilivyo
Azam FC kwani wao ndio mabingwa wa kihistoria wa iliyokuwa michuano ya
vijana ya timu za Ligi Kuu (Uhai Cup) baada ya kutwaa mara nne huku pia
ikitwaa ubingwa wa vijana wa Rollingstone mwaka 2014.
Azam Academy pia imetwaa taji la kwanza la michuano ya Azam Youth Cup
lilioanza mwaka huu baada ya kuzishinda timu nne shiriki, Football For
Good Academy (Uganda), Ligi Ndogo Academy (Kenya) na Future Stars
Acedemy (Arusha).
Kuhusiana na makocha waliowahi kuinoa Azam FC, mpaka sasa ni watano,
ambao ni Mzawa Mohamed Seif ‘King’, Mbrazil Neider Santos, Itamar
Amorin, Mwingereza Stewart Hall, Mcameroon Joseph Omog na Zeben
Hernandez kutoka Hispania ambaye amekabidhiwa timu hiyo hivi sasa kwa
ajili ya msimu ujao (2016-2017).
No comments:
Post a Comment