Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF),
Theophil Makunga kutokana na kifo cha Joseph Senga – Mpigapicha Mkuu wa
Gazeti la Tanzania Daima.
Rais Malinzi amepokea taarifa za kifo cha mwandishi huyo mwandamizi
wa habari aliyebobea kuripoti habari za aina mbalimbali ikiwamo za
michezo nchini kilichotokea jioni ya Julai 27, 2016 huko India,
alikokuwa akipatiwa matibabu ambako habari za kifo chake zilianza
kusambaa usiku wa kuamkia jana Julai 28, 2016 kabla ya kuthibitishwa na
Mhariri Mtendaji wa Free Media, Neville Meena.
Salamu za rambirambi za Rais wa TFF Malinzi pia zimekwenda kwa
familia ya marehemu Joseph Senga, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka
kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.
Malinzi alimwelezea Joseph Senga, wakati wa uhai wake alikuwa na
mchango mkubwa katika tasnia ya habari za michezo akitoa mawazo yake
hivyo ameacha alama ya ucheshi, kujituma na uwajibikaji katika
kufanikisha kazi zake katika gazeti la Tanzania Daima na wakati fulani
magazeti ya Kampuni ya New Habari House 2006.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Joseph Senga mahala pema peponi.
Bwana alitoa, Bwana alitoa, jina la Bwana lihimidiwe.
No comments:
Post a Comment