Dodoma. Wakati Rais Jakaya Kikwete akikutana na
viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD) ili kuzungumzia mchakato wa Katiba, Jukwaa la Wakristo Tanzania
(TCF), limesema amani ya nchi iko mikononi mwa kiongozi huyo mkuu wa
nchi.
Kwa maana hiyo viongozi wa vyama vya siasa hasa
vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanatarajiwa
kusafiri hadi Dodoma kumfuata Rais Kikwete ambaye leo anaingia katika
siku ya tatu ya ziara yake mkoani hapa, iliyoanza juzi katika Wilaya ya
Kongwa.
Baadhi ya viongozi ambao wanatarajiwa kushiriki
mkutano huo ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia.
Pia katika orodha hiyo wamo Mwenyekiti wa TCD
ambaye pia ni Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Mwenyekiti wa TLP,
Augustine Mrema na mwakilishi wa vyama visivyo na wabunge ndani ya TCD
ambaye pia ni Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa. Ukiondoa Kinana,
viongozi wengine ni wajumbe wa Bunge Maalumu.
Habari zilizopatikana juzi na jana Dar es Salaam
na Dodoma na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva
Rweyemamu zinasema mkutano huo umepangwa kufanyika leo jioni baada ya
Rais Kikwete kuhitimisha ziara yake katika Wilaya ya Chamwino na unaweza
kuendelea hadi usiku kutokana na jinsi ratiba ilivyokaa.
“Mkutano utafanyika hapa Dodoma katika muda wa
saa 48 kuanzia sasa na Rais hatakutana na Ukawa kama ambavyo imekuwa
ikidaiwa, anakutana na viongozi wa vyama vya siasa,” alisema Rweyemamu
jana mchana alizpoungumza na gazeti hili.
Mwanzoni mwa wiki hii, Cheyo aliwaambia waandishi
wa habari mjini Dodoma kuwa Rais Kikwete alikuwa amekubali kukutana na
viongozi wa vyama vya siasa wiki hii ili kuzungumzia mustakabali wa
Katiba. Hata hivyo, alipoulizwa jana siku ya mkutano pamoja na mahali
utakapofanyika, Cheyo hakuwa tayari kuzungumza chochote.
Mkutano huo wa Rais na viongozi hao umekuja
wakati ambao kamati za Bunge Maalumu zimekamilisha uchambuzi wa Rasimu
ya Katiba, bila kuwapo kwa wenzao wanaokaribia 120 ambao walisusia
mchakato huo tangu Aprili 16, kutokana na kile walichodai kuwa ni
kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda.
Mara kadhaa Ukawa wamesisitiza kwamba kamwe
hawatarejea bungeni hadi pale masharti yao yatakapotekelezwa na CCM
kikishikilia msimamo wake kwamba masuala yote yanayohusu Katiba Mpya
lazima yatatuliwe ndani ya Bunge. Kwa kuzingatia mazingira hayo ni
dhahiri kwamba matokeo ya kikao hicho yanasubiriwa kwa shauku kubwa
kwani yanaweza kusaidia kukwamua mchakato wa Katiba ambao umekosa
uhalali wa kisiasa kutokana na Ukawa kuususia.
Mzigo wa amani
Wakati hayo yakiendelea Jukwaa la Wakristo
Tanzania (TCF) limetoa tamko kali kuhusu mchakato wa Katiba, na likiweka
bayana kwamba ni Rais Kikwete pekee ambaye anaweza kukwamua suala hilo.
Jukwaa hilo linajumuisha taasisi kubwa za
madhehebu ya Kikristo ambazo ni Baraza la Maaskofu Katoliki nchini
(TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya
Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA.)
“Tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba amani ya nchi yetu sasa imo
mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya,”
inasomeka sehemu ya tamko hilo lenye kurasa nne na kuongeza: “Tunakuomba
uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za
kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri
vibaya mshikamano, umoja na amani ya taifa letu.”
Tamko hilo ni matokeo ya mkutano wa siku mbili
uliofanyika Agosti 27 na 28, 2014 jijini Dar es Salaam ambako TCF pia
walimnyooshea kidole Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta kwamba
amekuwa akiendesha Bunge hilo kwa ubabe akijivunia wingi wa wajumbe
kutoka CCM.
“Maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na
kudharauliwa na chama tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba
linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba na siyo kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977,”
inasomeka sehemu nyingine ya tamko hilo.
TCF inapendekeza kusimamishwa kwa mchakato wa
Katiba ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano yatakayowezesha
kurekebishwa kwa Katiba ya sasa kwa lengo la kujenga mazingira bora ya
Uchaguzi Mkuu ujao na ule wa Serikali za Mitaa.
Lilisema wakati Bunge hilo likiwa limesimamishwa,
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifanyiwe marekebisho ili kumbana Rais
ajaye kuendelea na mchakato huo baada ya kuwa maridhiano yamepatikana.
“…Baada ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza
shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa
kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na
kiburi cha wingi wa wajumbe wa CCM katika Bunge hilo,” inasomeka sehemu
nyingine ya tamko.
Chanzo Mwananchi.
Chanzo Mwananchi.
No comments:
Post a Comment