Geita. Hatimaye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa matokeo ya sampuli zilizopelekwa Nairobi nchini Kenya, kubaini chanzo cha utata wa kifo cha Bertha
Boniphace (25) aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Geita, mkoani
hapa baada ya kuenea uvumi kuwa alikuwa akiumwa ugonjwa wa ebola.
![]() |
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dkt. Seif Rashid |
Akizungumza kuhusu matokeo ya sampuli hizo jana,
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk Adam Sijaona alisema
matokeo kutoka Nairobi yanaonyesha Bertha hakuwa na ugonjwa wa ebola bali alikuwa anaumwa ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama Chikungunya Viral Hemorrhagic Fever (VHF).
“Matokeo yametoka rasmi hakuuawa na ugonjwa wa
ebola kama tulivyozungumza awali ila unaelekea kwenye kundi la ebola,
dengue na homa ya bonde la ufa. Ni ugonjwa wa kitropiki. Kitaalamu
tunauita Arthropod borne virus, unaenezwa na mbu aina ya Aedes Aegyti,” alisema Dk Sijaona na kuongeza:
“Aina hii ya mbu ni wachache na wanapatikana
kwenye maeneo yenye unyevuvyevu kama wengine, Bertha alikuwa akifanya
kazi maeneo ya madini Kata ya Katoro ambako mbu hao ni rahisi
kupatikana.
“Lakini siyo ugonjwa wa kawaida nchini ingawa siyo
hatari kama virusi vya ebola. Ni kesi chache za aina hii kwa sababu
tangu apatikane huyu hadi leo hakuna mgonjwa mwingine aliyeripotiwa, ila
watu wanatakiwa kuchukua tahadhari.”
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Joseph Kisala alisema ugonjwa huo ni mpya nchini na kwamba, haujazoeleka barani Afrika na kama ilivyo kwa magonjwa ya VHF hauna tiba maalumu.
Dalili zake
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), aina ya magonjwa ya VHF yana tabia ya homa za mara
kwa mara, mwili kudhoofika, kutokwa na vipele vidovidogo mwili mzima,
kutokwa damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani na masikioni na kwamba
dalili hizo ni kama za dengue.
Bertha Boniphace (25) alifariki dunia Agosti mwaka
huu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, huku kifo chake kikisababisha
uvumi kuwa alikuwa anaumwa ebola hatua iliyosababisha uongozi wa mkoa
kukanusha uvumi huo.
Mgonjwa huyo alitokea Kata ya Karoro-Buserere
akisumbuliwa na kutapika, kuharisha damu na kutoka damu sehemu za mdomo
na puani, dalili ambazo zinashabihiana na zile za ugonjwa wa Ebola hali
iliyosababisha watu kufikiria kuwa ameuawa na ugonjwa huo.
Kutokana na utata huo, uongozi wa hospitali
ulichukua tahadhari muhimu kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo huku ukikataa
kutoa mwili kwa ndugu zake kwenda kuuzika na kuchukua jukumu la mazishi
hayo.
Chanzo Mwanachi
Chanzo Mwanachi
No comments:
Post a Comment