Kundi la
wanamgambo wa Al Shabab limetangaza kumchagua kiongozi mpya wa kundi
hilo kufuatia kuuawa kwa kiongozi wao Ahmed Abdi Godane katika
shambulizi la anga lililotekelezwa na wanajeshi wa Marekani mjini
Mogadishu siku ya Jumatatu.
Pia kundi hilo limeapa kulipiza kisasi kwa kifo cha kiongozi
wao na kusema kwamba litaendeleza mashambulizi yao kuiangusha serikali
ya Somalia inayoungwa mkono na mataifa mbalimbali duniani.
Taarifa ya kundi hilo iliyochapishwa kwenye mtandao wa jihadi na
kuthibitishwa na maafisa wa kundi hilo imetolewa baada ya serikali ya
Somalia kuonya kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kisasi kutoka kwa
kundi hilo.
Serikali ya Somalia imeonya kuwa huenda nchi hiyo ikakumbwa na wimbi
la mashambulizi ya kisasi ya wanamgambo wa Al Shabab baada ya kiongozi
wao kuthibitishwa kuuawa kwenye shambulizi la anga lililotekelezwa na
Marekani.
Rais wa nchi hiyo ya pembe ya Afrika pia amewapa nafasi wanamgambo wa
Al Shabab kuweka silaha zao chini na kuachia maeneo wanayoshikilia kwa
msamaha wa siku 45, akiwaambia kwamba vikosi vya serikali na vya Umoja
wa Afrika AMISOM wakombioni kuvamia maeneo yao.
Siku ya Ijumaa Marekani imethibitisha kuuawa kwa kiongozi wa
wanamgambo hao wa al-Shabab, Ahmed Abdi Godance, katika shambulizi
lililotekelezwa na wanajeshi wake mapema siku ya Jumatatu.
Chanzo RFI
No comments:
Post a Comment