![]() |
Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele akihutubia wakazi wa Tanga katika mkutano wa ACT uliofanyika hapo jana |
Akieleza furaha zake kwa wana Tanga Zito Kabwe amesema kuwa ana furaha kubwa mno kuwa hapa Tanga huku furaha yake ikitokana na mambo mawili makuu.
Mosi: Ni kuzileta Tanga harakati mpya za Siasa za Kizalendo nchini, Siasa za kuirudisha nchi yetu katika misingi yake, Siasa za Chama chetu cha ACT Wazalendo.
Furaha yangu kwenye hili ni kuwa nimezileta Siasa hizi pahala penyewe sahihi, kwa watu watanga, watu wazalendo na wenye fasaha ya matamshi. Jambo hili la harakati za Siasa za Kizalendo kuletwa Tanga si geni kwenu, maana hata historia ya Ujenzi wa Taifa letu inaonyesha hivyo.
Ni harakati za Wazalendo wanaTanga Wazee wetu Stephen na Peter Mhando, Mwalimu wa Mwalimu wa Kihere, Makatta Mwinyimtwana, Bakari Maharage Juma Mwawado, Chifu Erasto Mang'enya, Hamza Kibwana Mwapachu, Rashid Sembe na Hamisi Heri Ayemba kuziingia Siasa za Ukombozi za Taifa hili kuanzia Chama cha TAA na kisha TANU ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa zilisaidia kuleta Uhuru wa Tanganyika.
Tanga kilikuwa kitovu cha Uchumi wa Tanganyika, kuanzia Mashamba ya Mikonge mpaka viwanda vidogo, Harakati za wanatanga kuipokea TAA na kisha TANU zilisaidia sana kuharakisha kupatikana kwa Uhuru wetu.
Hivyo sisi katika ACT tumeamua kurudi kwenye misingi, kukileta kwenu Wanatanga Chama chenu hiki cha ACT Wazalendo, ili kama ilivyo ada mzibebe harakati hizi za kurudisha Uzalendo wa Taifa hili.
Sababu ya Pili ya Furaha yangu, ni kwa kuwa nimelileta kwenu Azimio la Tabora, Muongozo wa Kimaadili, Kiuongozi, Kisera na Kiitikadi wa Chama chetu, Muongozo unaohuisha Azimio la Arusha.
Nina furaha kwa kuwa asili ya Azimio hili la Tabora mzizi wake ni Tanga, mzizi wake umejengwa katika kuenzi Mchango wa Mzee wetu wa hapa Tanga, Mwalimu wa Mwalimu wa Kihere, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano uliofanya Uamuzi wa Busara wa Tabora wa 1958 wa Chama cha Tanu.
Hapa Tanga kuna mgahawa unaitwa Patwas, uko mjini pale katika jengo lililo katikati ya Majestic Cinema na Jengo la Bora, mgahawani pale zipo Picha za mwaka 1957, zikimuonyesha Mwalimu Nyerere akifanya hiki ambacho ACT Wazalendo tunakifanya Tanga, kuzikabidhi harakati za Siasa za Kizalendo kwa wenyewe hasaaa, Wanatanga.
Tumekuja Tanga kutambulisha chama chetu cha ACT.
Hata Hivyo Zito Kabwe pia amesikitishwa kwake kuitwa msaliti na baadhi ya viongozi na kuwataka watanzania wasimuhukumu kupitia midomo ya watu bali wamuhukumu kupitia utendaji wake wa kazi wakati yupo Bungeni.
No comments:
Post a Comment