BUNGE la 10 linamaliza shughuli zake leo kabla ya Rais Jakaya Kikwete
kulihutubia na kulivunja mjini Dodoma. Rais atalihutubia Bunge hilo saa
10:00 jioni baada ya kukagua gwaride la heshima, lililoandaliwa na Jeshi
la Polisi katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
![]() |
Rais Jakaya Kikwete |
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge jana baada ya
kukagua gwaride, Rais Kikwete atakwenda ukumbi maalumu wa Spika, kusaini
kitabu cha wageni kabla ya kuingia ukumbini na kuhutubia.
Anatarajiwa kutoka katika ukumbi huo wa bunge saa 12:15 jioni, baada
ya kuhitimisha shughuli za bunge hilo.
Miongoni mwa viongozi
watakaohudhuria shughuli hizo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dk Gharib Mohammed Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohammed Shein.
Wengine ni marais wastaafu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mohammed Chande Othman.
Wakati Bunge hilo likifika ukomo wake, wabunge wa vyama vya upinzani
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesusa kuhudhuria
kikao cha leo wakati Rais atakapohutubia kwa mara ya mwisho.
Wabunge hao walifikia uamuzi huo kwa madai kuwa Serikali imepitisha
miswada mitatu ya sheria, inayohusu petroli na gesi, kinyume cha kanuni.
Wakipinga upitishwaji wa miswada hiyo, wabunge hao wa upinzani
walifanya vurugu zilizosababisha wabunge 35 kusimamishwa kuhudhuria
vikao kuanzia viwili hadi vyote vilivyosalia.
Adhabu hizo zilitolewa na Kamati ya Maadili ya Bunge na uamuzi wa
Spika kutumia mamlaka yake. Wakati Chadema ni miongoni mwa wana Ukawa,
ambao leo hawahudhurii kuvunjwa kwa bunge hili, vile vile wakati Bunge
likizinduliwa Novemba 2010, wabunge wa chama hicho pia walisusa kwa
madai ya kutomtambua rais, ingawa baadaye walitengua msimamo huo.
CHANZO HABARI LEO
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment