BAADA ya mchuano wa kuwania uteuzi wa kugombea urais wa Tanzania kwa
tiketi ya CCM uliomalizika kwa Dk John Magufuli kuibuka mshindi, kwa
wiki moja kuanzia leo joto la siasa linatarajiwa kuhamia kwa makada wa
chama hicho wanaowania kuteuliwa kuwania ubunge na udiwani kote nchini.
Chama hicho tawala, kinatarajiwa kuanza kutoa fomu za ubunge, udiwani
na wagombea wa Ujumbe katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kutokana
na kufunguliwa kwa pazia hilo, wananchi wenye sifa za uongozi
wamehamasishwa kujitokeza.
Kwa mujibu wa ratiba ya mchakato wa uteuzi ndani ya CCM, fomu hizo
zitakazogharimu Sh 100,000 kwa wagombea wa ubunge na Sh 10,000 kwa
upande wa madiwani, zitatolewa hadi Julai 19, mwaka huu.
Kwa upande wa Dodoma Mjini, akizungumza na gazeti hili jana Katibu wa
CCM wilaya hiyo, Albert Mgumba alisema mkoa wa Dodoma umejipanga vizuri
katika kuhakikisha zoezi hilo linakwenda vizuri.
Alisema fomu zitakazotolewa kuanzia leo ni zile za Udiwani na Udiwani
Viti Maalumu huku zile za Ubunge zikiwa na za Ubunge wa Jimbo na Ubunge
Viti Maalumu. Alitoa wito kwa wana CCM kujitokeza kwa wingi kuchukua
fomu ili kutimiza haki yao ya kuchaguliwa.
“Tunahimiza wanawake kwa vijana kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu,” alisema.
Alisema CCM mkoa wa Dodoma imefanya uhamasishaji wa kutosha kuanzia
vikao vya ndani na hata vikao vya nje kwenye mikutano ya hadhara ambapo
wananchi wamehamasishwa kujitokeza kuchukua fomu.
Mgumba alisema baada ya kumalizika kwa zoezi la uchukuaji fomu, Julai
20, mwaka huu kampeni matawini zitaanza na kumalizika Julai 31, mwaka
huu. Alisema kura za maoni kwenye matawi zitafanyika Agosti Mosi mwaka
huu.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment