Home Traders

Home Traders

Tembelea TK FM Redio 88.5 Tanga

Saturday, 30 July 2016

Majengo ya Serikali Kupigwa Mnada

WAKATI suala la serikali kuhamia mkoani Dodoma likiwa dhahiri zaidi kila siku moja inayoongezeka, Rais John Magufuli ametangaza kuuza majengo ya wizara Dar es Salaam, mara atakapohamia yeye katika makao makuu hayo ya nchi.
Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara mkoani Singida, katika siku ya kwanza ya ziara yake itakayomfikisha mikoa minne, Rais Magufuli alisema atahakikisha anauza baadhi ya majengo hayo kwa mnada, ili wale wasiotaka kuhama, wahame kwa lazima.
Rais Magufuli amesema majengo atakayoanza nayo, ni yale yanayotazama bahari; ambayo ndiyo mazuri zaidi, yenye mwonekano mzuri kutoka ofisini.
Mbali na Singida, mikoa mingine atakayotembelea katika ziara hiyo aliyoanza jana ni Tabora, Shinyanga na Geita, ambako atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Katika mikutano hiyo, Rais Magufuli anatarajiwa kushukuru wananchi kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali kutatua kero zao na kuwaletea maendeleo.
Uamuzi huo wa serikali kuhamia Dodoma japo ni wa siku nyingi na utekelezaji wake ulikuwa ukifanyika kidogokidogo kwa baadhi ya wizara na ofisi nyeti kujenga majengo yake katika mji huo, lakini hivi karibuni umepata kasi ambayo haijawahi kupatikana, baada ya Rais Magufuli kutangaza kuhakikisha serikali yote inahamia Dodoma kabla ya 2020.
Tamko hilo la Rais Magufuli lililotolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM wiki iliyopita na kurejewa katika Sikukuu ya Mashujaa mwanzoni mwa wiki hii, liliungwa mkono mara moja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye alitangaza kuharakisha umaliziaji wa ujenzi wa nyumba yake, ili ahamie katika mji huo Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment