Zanzibar. Madai ya Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kuingia katika kinyang’anyiro cha urais yameibua mjadala mkali
kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, wasomi na wananchi wa Zanzibar ambao
wamesema hafai kutokana na kauli yake kuwa ‘Zanzibar si nchi’.
Wakizungumzia uamuzi huo ulioripotiwa na vyombo vya habari juzi, baadhi ya wananchi hao wamempinga na wengine kumuunga mkono.
Aliyekuwa mgombea mwenza wa TLP katika Uchaguzi
Mkuu 2010, Abdallah Othman Mgaza alisema Pinda anaponzwa na kauli yake
kuwa Zanzibar si nchi... “Zanzibar ni nchi kamili ndani ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kwa kutojua kwake akasema si nchi na kuwakera
Wazanzibari. Anapoteza muda wake bure kwa kufikiria urais wa Muungano,
sehemu moja ya dola hawana imani naye.”
Mwanasiasa mkongwe Zanzibar, Soud Mwana Nassor
(74) alisema katika uchaguzi ujao, Watanzania wanahitaji rais awe
kiongozi mwenye sauti itakayosikilizwa na wananchi, mwenye uwezo wa
kusimamia uamuzi wake na asiwe na makundi wala upendeleo katika
uendeshaji wa Serikali.
“Napata taabu kusikia majina yanayotajwa hivi sasa
ya wanaotaka urais, hata zile mamlaka walizokabidhiwa wazisimamie
zimewashinda,” alisema Soud ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa UDP
Zanzibar.
Mkurugenzi wa Uenezi, Habari na Mawasiliano kwa
Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani alisema chama hicho kimepata mshangao
kusikia Pinda akitaka kuwamo katika orodha ya wanaojitaja kuwania urais
wa Muungano wakati upande mmoja wa Muungano bado una kinyongo naye kwa
matamshi yake yaliyodai Zanzibar si nchi.
“Ndugu zetu CCM Zanzibar wana kawaida ya
kutotusikiliza na kutubeza, kwa hili tunawaomba chondechonde wafungue
masikio yao, akiwa waziri mkuu alisema Zanzibar si nchi, akipata urais
ataitangaza nchi yetu mkoa na kutuletea gavana mkaazi,” alisema Bimani.
Hata hivyo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM,
Wilaya ya Mjini, Baraka Mohamed Shamte alisema kitendo cha Pinda
kujitokeza mapema ni mwafaka na kitasaidia watu kumpima, kumchambua na
kuainisha sifa zake kabla ya kuchukua fomu na taratibu za vikao vya CCM
kufanyika.
“Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kupata dola
moja, nje ya nchi Zanzibar si nchi, ndiyo maana hata katika kesi ya
uhaini iliyowakabili wanachama 18 wa CUF Mahakama ilitamka Zanzibar si
nchi na hakuwezi kufanyika uhaini,” alisema Shamte.
Alisema wanaomponda Pinda kwamba ni dhaifu
wanashindwa kuelewa kama yeye ni waziri mkuu chini ya Rais anayetawala
dola na si mwamuzi wa mwisho katika usimamizi wa masuala ya kiutawala.
Mwanasheria, Omar Makame alisema suala la Pinda
kutaka urais wa Muungano litaamuliwa na wakati ingawa wanasiasa wengi
wanaotajwa kuwania nafasi hiyo bado hawajawekeza na kukubalika ipasavyo
upande wa pili wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment