Dar es Salaam.Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
amesema CCM ndiyo iliyomsukuma kwenda upinzani kama inavyofanya sasa kwa
aliyekuwa kada wake, Mansour Yusuf Himid.

"Mimi sikuamua kuja upinzani, CCM
ilinisukuma kama anavyopitia Mansour sasa hivi. Kweli Mansour anapitia
vilevile nilivyopitia. Nilifukuzwa CCM, ilitafutwa tu sababu nikakamatwa
na kuwekwa ndani. Mansour naye hakutoka CCM, wamemfukuza," alisema
Maalim Seif.
Mansour ambaye kabla ya kutimuliwa CCM
alikuwa waziri asiye na wizara maalumu na Mwakilishi wa Kiembesamaki,
alivuliwa uwaziri na baadaye uanachama kwa madai ya kukisaliti chama
hicho.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu
wa Chama cha Wananchi (CUF) alisema bado Mansour hajajiunga na upinzani,
lakini hutoa mchango wake wa mawazo katika majukwaa yake.
"Baada ya kufukuzwa akaona watu walio
karibu na msimamo wake ni CUF. Hajajiunga rasmi mpaka leo lakini huja
kwenye mikutano yetu kujieleza. Sasa wamemtia ndani, ipo siku watamtoa,"
alisema Maalim Seif na kuongeza:
"Lakini 'they are making him a hero,
they create heroes themselves' (wanamfanya awe shujaa, wanatengeneza
mashujaa). Nakumbuka Mwalimu Nyerere (Julius) aliwahi kuulizwa na Sauti
ya Ujerumani kwamba mambo gani anayojutia katika uongozi wake. Moja
alisema ni kuitambua Biafra na jambo la pili ni kuwafukuza kina Maalim
Seif."
Akifafanua zaidi jinsi alivyofukuzwa
kutoka CCM, Maalim Seif alisema Mwalimu Nyerere alifuata ushauri wa
Idara ya Usalama wa Taifa ya Zanzibar ambayo ilimtaka Seif na wenzake
wafukuzwe mara moja, huku idara hiyo upande wa Bara ikimwonya Mwalimu
kutochukua hatua hiyo.
"Kikao cha Dodoma kilichoitishwa,
kilikwenda mpaka saa sita usiku maana siku inayofuata Mwalimu alikuwa
anasafiri na ilikuwa ni lazima tufukuzwe tu. Utetezi tulioutoa, hata Job
Lusinde na marehemu Jamal walisema 'mnawaonea tu vijana hawa, hawana
kosa lolote'," alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya kufukuzwa
alijiona kuwa yuko huru zaidi, huku akifungua ukurasa mpya wa kuwa nje
ya uongozi wa Serikali.
"Kufukuzwa kwangu hakukuniuma, kwani
nilijiona nitakuwa huru kufanya mambo yangu na hasa nilipoona ninaungwa
mkono na Wazanzibari. Nilijiona kama nimepata baraka ya kuwa huru,
wamenitesa, lakini nikaona ni mapambano, hakuna kukata tamaa," alisema.
Alipoulizwa iwapo ana mpango wa kurudi CCM siku za usoni, Maalim Seif alihoji:
"CCM? Hii ya kina Nape? Afadhali ile
yetu sisi ya enzi hizo. Kwa kweli haiwezekani. CCM ilikuwa ile ambayo
Mwalimu ni Mwenyekiti, Kawawa (Rashidi) ni Katibu Mkuu, kina Kingunge
(Ngombale Mwiru), Moses Nnauye, Salim Ahmed Salim, Alfred Tandau, ndiyo
iliyokuwa sekretarieti. Siyo CCM hii... Kwa nini hasa nijisumbue kurudi
CCM wakati chama chetu kinaendelea kuimarika?" alihoji.
Akanusha kumsaliti Jumbe
Kuhusu suala la kutofautiana na Rais
wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Aboud Jumbe ambapo Maalim
Seif anadaiwa kumsaliti katika Halmashauri Kuu ya CCM hadi akaondolewa
kwenye nafasi ya urais mwaka 1984, Maalim Seif amesema siyo kweli.
"Mimi sikupinga Serikali tatu. Wakati
ule, Wazanzibari katika chama tuligawanyika. Kuna wale wazee (waasisi)
wakijiita 'Liberators' kwa maana ndiyo walioleta mapinduzi, wakati huo
mimi ni kijana. Hata Aboud Jumbe alipoleta Katiba ya mwanzo waliipinga.
Lakini sisi vijana tukijiita 'Front liners' tulimuunga mkono," alisema
na kuongeza:
"Hata katika kugombea nafasi za Nec
kulikuwa na makundi, haya yalikuwa yanagombana. Liberators walitaka sisi
vijana tusiiingie kwenye Nec. Hata hivyo, walikuta vijana wamekuwa
wengi zaidi. Hii iliwashtua Liberators.
"Wakahisi hawa vijana watachukua
madaraka yao. Walimlaumu sana Jumbe kutuingiza kwenye madaraka, sisi
tulimsaidia Jumbe kupitisha Katiba. Sasa fitina zikaanza, wanasema
Waswahili papo kwa papo."
Kutokana na uhasama huo wa makundi,
Maalim Seif alisema kundi la Liberators lilizusha uongo kuwa amemsaliti
Jumbe kwa kukataa Serikali tatu:
"Baada ya kutokea uchaguzi mkuu wa
chama, Jumbe akaitisha kikao cha Unguja na Pemba mjini Dodoma. Katika
hotuba yake ndiyo ilitushtua kwani alizungumzia muungano na mgawanyo.
Mwisho akasema tunakwenda kwenye 'revolutionary justice' (mapinduzi ya
haki). Hiyo ilitushtua maana tulishaona watu wakipoteza maisha," alisema
na kuongeza:
"Sasa mimi, Dk Salim Amour, Salim
Ahmed Salim, wakati huo ni wajumbe wa Nec, tutachukua majukumu kwa
upande wa Zanzibar. Tujue maana ya hii 'revolutionary justice'. Tukaenda
kwenye sekretarieti ya chama tukalijadili.
"Sasa kwa sababu Liberators
walishindwa kutuzuia, ndipo walipokuja na suala la serikali tatu
kutuengua. Nakumbuka hata marehemu Sokoine (Edward) alimwambia Mwalimu,
vijana hawa wakija kupoteza maisha utawajibika. Sokoine alikuwa wazi
sana, alikuwa Waziri Mkuu mwenye maamuzi na anayejiamini na mwenye
nguvu."
Maalim Seif alisema walilazimika
kumruka Jumbe kwa kuwa hakuwashirikisha kikamilifu katika mpango wa
mapinduzi aliyotaka kuyafanya:
"Kama kweli Jumbe alikuwa anataka
mamlaka zaidi ya Zanzibar, sisi Wazanzibari wenzake kwa nini hakutuita
walau tujadili na tuwe sehemu ya madai hayo, ili tukija kwenye Nec tuwe
pamoja? Anafanya chini kwa chini? Kwa nini?"
Msimamo kuhusu Muungano
Maalim Seif amesisitiza msimamo wake
katika muundo wa muungano kuwa ni Serikali ya mkataba. Hata hivyo, licha
ya muundo huo kutoingizwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, anasema bado
ameheshimu uamuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
"Serikali ya Mkataba ni rahisi sana,
Tanganyika inakuwa na Serikali yake na Zanzibar Serikali yake. Kisha
mnakaa pamoja na kuangalia mambo gani mwendeshe pamoja. Jeshi, Polisi na
mambo mengine mnayoona kwa masilahi yenu kuyafanya pamoja," alisema na
kuongeza:
"Halafu siyo kuvunja muungano,
haiwezekani leo kusema muungano usiwepo kabisa. Miaka 50 hii siyo
michache, watu wamefanya mengi, wameshaoana sana. Lakini Wazanzibari leo
wamebanwa, koti la muungano limetubana sana. Sasa tunataka tupime ili
tupate koti ambalo haliwabani Tanganyika wala Zanzibar."
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment