UONGOZI
wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), pamoja na wamiliki wa
daladala mkoa wa Dar es Salaam, wamesaini mkataba wa makubaliano ya
kushirikiana kwa lengo la kushinda zabuni ya kuendesha mradi wa mabasi
yaendayo haraka (DART) jijini Dares Salaam.
Utiaji saini huo, ulifanyika jijini DaresSalaam mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa
mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kushuhudiwa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Hawa Ghasia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadiki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ghasia alisema uamuzi
uliyochukuliwa na UDA na wamiliki wa daladala ni mfano wa kuigwa nchini.
Alisema kuungana kwao pamoja, kutawajengea mazingira bora ya
kuaminika zaidi, ambayo yatatoa ushindani madhubuti dhidi ya kampuni za
nje zitakazojitokeza kuomba kuendesha mradi wa DART.
Pia, alimpongeza Mwenyekiti wa Saimon Group, Robert Kisena na
viongozi wa vyama vya wamiliki wa daladala Mkoa wa Dar es Salaam kwa
uamuzi huo wenye tija kwa taifa, kwani utaongeza ajira zaidi na
kupunguza umasikini.
Uamuzi huo, ulifikiwa baada ya mkutano wa mafanikio uliyofanyika
Ijumaa iliyopita kwenye ukumbi wa Karimjee ulioandaliwa na kamati teule
ya wamiliki wa daladala jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wamiliki
wote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadiki, alisema kuunganisha
nguvu kwa wadau hao kutatoa fursa kwa serikali kuwaunga mkono katika
jitihada zake za kuboresha hali ya usafiri Dar es Salaam.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Saimon Group inayomiliki UDA, Robert
Kisena, alisema watafungua milango kwa wamiliki hao kununua hisa
zitakazowezesha mtu yeyote kuwa mkurugenzi.
“Pia tunatoa wito kwa wananchi mbalimbali kujitokeza kununua hisa kwa
wingi zaidi ili kuhakikisha tunaboresha huduma ya usafiri katika jiji
hili,” alisema Kisena.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Darcoboa, Sabri Mabrouk, alisema
kutokana na UDA kuwa kampuni yenye uwezo, kuna haja ya kuunganisha nguvu
kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba zabuni itakapotangazwa hakuna kampuni
kutoka nje itakayoshinda.
No comments:
Post a Comment