Dodoma. Kauli ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta
kwamba fedha ambazo zitakuwa zimeokolewa katika siku 60 za uendeshaji wa
Bunge hilo hazitarejeshwa serikalini, bali zitatafutiwa utaratibu wa
namna ya kuzitumia, imemgonganisha na katibu wake, Yahya Khamis Hamad
ambaye amesema “hilo ni jambo la ajabu”.
Sitta alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati
akiahirisha Bunge hilo lenye wajumbe 500 baada ya wajumbe 130 wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kulisusia tangu Aprili 16, mwaka huu.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh300,000
kwa siku sawa na Sh150 milioni kwa siku kwa wajumbe wote, huku Serikali
ikiwa imetenga Sh20 bilioni kwa ajili ya siku 60 za uendeshaji wa Bunge
hilo.
Kauli hiyo ya Sitta kuwa fedha zitakazookolewa
zitatafutiwa utaratibu badala ya kurudishwa zilikotoka, iliwafanya
wajumbe wa Bunge hilo kulipuka kwa furaha na kugonga meza.
Hata hivyo, katibu wa Bunge, Yahya Khamis Hamad
alishangazwa na kauli hiyo ya Sitta akisema: “Mimi hayo niliyasikia
lakini kwangu pia ni ya ajabu kwa sababu fedha tulizonazo hazitoshi,
sasa hizo za kubaki mimi sijui.”
Katibu huyo alisema kwa sasa, Wizara ya Fedha
inawapa kiasi cha fedha kwa kile tu ambacho kinahitajika na yeye anatoa
taarifa serikalini kwa kiasi kilichotumika. “Mimi sijui labda yeye
anajua sitaki kumsemea,” alisema.
Sitta pia aliwaeleza wajumbe hao kuwa baada ya
kukabidhi Katiba inayopendekezwa, wote watakabidhiwa cheti na Rais
Jakaya Kikwete.
“Cheti hicho kitakuwa na sahihi ya Rais mwenyewe
kwa hiyo tutakaa kidogo kusubirisubiri Katiba iliyokamilika, haiwezi
kuwa ya ovyo ovyo tu lazima iwe na viwango vizuri,” alisema Sitta na
kuongeza:
“Tutachapisha nakala nyingi kila mmoja aende na
waraka huo wa kihistoria nyumbani na itakuwa ni Katiba bora sana hapa
Afrika na Kusini mwa Sahara.”
Mwenyekiti huyo aliwapiga vijembe viongozi wa
Ukawa na makundi mengine yanayopaza sauti kutaka Bunge hilo lisitishwe
ili kuokoa pesa
“Tutamaliza zoezi hilo Oktoba 3, mwaka huu ili
tutoke na Katiba inayopendekezwa kinyume na wale wanaopiga kelele ovyo
bila kuwa na sayansi kichwani eti unaokoa gharama kwa kusitisha
mchakato.
“Mchakato huu ungesitishwa ina maana utawala ujao,
rais ajaye ingembidi kuanza upya na Tume na aingie tena kwenye Bunge
Maalumu la Katiba,” alisema Sitta.
“Lakini tukiwa na Katiba inayopendekezwa basi hilo ni tunda
lililoiva atakabidhiwa Rais ajaye apeleke kwenye kura ya maoni na kazi
itakuwa imekwisha na nchi inaendelea na kazi za maendeleo.
“Hapo ndiyo tunataka tufike. Tukabidhi kitu
kilichokamilika, gharama yote iliyotumika tangu Tume ya Warioba (Joseph)
na Bunge Maalumu itakuwa sasa imepata majibu, hakuna kilichopotea kwa
sababu sasa tutakuwa tumeshapata Katiba inayopendekezwa.”
Mchakato wa Katiba mpya, unaelezwa kutafuna fedha
nyingi za walipakodi huku iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ikielezwa kutumia Sh69 bilioni.
Mbali na matumizi hayo, Bunge la Katiba lililoketi
kwa siku 67 kuanzia Februari hadi Aprili mwaka huu lilitumia zaidi ya
Sh27 bilioni wakati Bunge la sasa limetengewa Sh20 bilioni.
Matumizi hayo ni pamoja na Sh8.6 bilioni
zilizotumika kukarabati ukumbi wa Bunge, miundombinu yake, mfumo wa
sauti na ule wa usalama.
Hofu ya theluthi mbili
Wakati Bunge hilo likiwa katika hatua ya lala
salama, kumeibuka hofu ya kupatikana au kutopatikana kwa theluthi mbili
za kupitisha Katiba inayopendekezwa.
Kutokana na hofu hiyo, Sitta amewataka mawaziri na manaibu kuwapo bungeni kuanzia Septemba 29.
Abadili kanuni
Sitta alisema ikiwa wajumbe watafuata kanuni za
Bunge hilo zinazotaka upigaji kura uwe ibara kwa ibara, shughuli hiyo
itachukua siku zisizopungua 300 kuwahoji wajumbe 460.
“Ibara naambiwa zinakaribia 300 kwa hiyo itachukua
siku moja kwa ibara moja. Na kwa ibara 300 ni siku 300; haiwezekani
kabisa ni kinyume cha sheria. Tumepewa siku 60 tumalize,”alisema Sitta.
Hivyo, alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge
imekabidhi suala hilo kwa Kamati ya Kanuni ili kuja na mapendekezo ya
njia bora ya kupiga kura hizo ili wajumbe wahojiwe sura kwa sura.
Dk Migiro
Awali, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Rose-Asha
Migiro alisema wajumbe waliosalia wanatosha kupitisha uamuzi kwa kuwa ni
halali kisheria na kisiasa.
Alisema wajumbe wote wa Bunge ni 630 na kati ya hao, waliotoka ni 130, idadi ambayo ni sawa na asilimia 21 tu ya wajumbe wote.
“Wajumbe waliobaki ndani ya Bunge ni 500 sawa na
asilimia 79 ya wajumbe wote na idadi hii ni pamoja na wajumbe 189 kutoka
Kundi la 201 ambao wamebaki Bungeni,” alisema.
“Wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati ya
hao 125 ni wanaotoka kundi la 201. Ukitazama takwimu zote hizi, wajumbe
wa 201 ni sehemu ya Bunge hili,” alisema Dk Migiro.
“Kwa Zanzibar wajumbe waliobaki ndani ni 152 na
kati ya hao 64 wanatokana na kundi la 201. Waliosusia Bunge kwa pande
zote za Muungano hawafikii theluthi moja ya wajumbe waliobaki.”
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment