MBUNGE wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala, amejitosa rasmi katika mbio
za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwaka 2015.
Tangazo hilo la Kigwangala, linaongeza idadi ya wanaowania kiti hicho
baada ya January Makamba, Bernard Membe, Edward Lowassa,William
Ngeleja, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza nia na
baadhi yao kutajwa kuwa na nia ya kufanya hivyo mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari, wazazi wake, familia yake na
makada wa CCM, akiwemo William Malecela (Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani
John Malecela), Dk. Kigwangala alitumia muda mrefu kufafanua hotuba yake
iliyokuwa na kurasa sita akielekeza kuwa, watanzania wanapaswa kubadili
mipangilio ya kipaumbele na kusimiamia mambo wanayoyasema ili
kujikwamua kiuchumi.
Kigwangala aliwaambia waandishi kuwa, anatangaza rasmi sasa, kuwa
anatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka
2015.
Alisema amefikia uamuzi huo bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa,
kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, isipokuwa utashi
utayari wake.
Bila kuwataja majina, Kigwangala aliponda njia wanazotumia wengine
akisema kuwa yeye hasubiri kuoteshwa, kushauriwa au kuombwa kama
wanavyofanya wagombea wengine kupitia CCM. Alisema baadhi ya wanasiasa
wa CCM, wamekuwa waoga kujitosa au kutangaza nia zao bali husema kuwa
wanasubiri kuoteshwa, au wengine wameombwa na watu wengine.
Alibainisha kuwa, anatangaza nia ya kugombea urais mapema ili kuwapa
fursa watanzania wampime na kumtazama mwenendo na uwezo wake, akiamini
kuwa ataungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yake, si kwa jinsi yake, si
kwa umri wake au kwa daraja lake kijamii, dini, ama kabila lake, bali
kwa sifa na uwezo wake kama mtanzania.
Kigwangala alitumia msemo wa kilatini kusema kuwa yeye ni baina ya
wengi, mmoja! (E Pluribus unum), hivyo hawezi kuwa salama ikiwa wengine
wanateseka.
Bila kutaja wazi kuwa anakosoa utendaji wa serikali ya Kikwete,
Kigawangala alitoa mifano mbalimbali ikiwemo kitisho cha njaa,
kucheleweshwa hukumu za mahakamani, shida za mzee mmoja wa Pemba
aliyefiwa na mtoto wake, au kasoro za operesheni za wamachinga na
mamantilie jijini Dar es Salaam.
“Kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani
Meatu, ni kitisho changu na familia yangu, hata kama siyo familia yangu.
Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule
Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu,” alisema.
Aliongeza kuwa Mama Ntilie wa Sokoni Kariakoo, akifukuzwa, akapigwa
virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula
chake na mgambo wa Jiji la Dar es Salaam inaniumiza na kunigusa moyoni,
hata kama yeye si mama yangu,” alisema.
Chanzo Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment