Dodoma/Dar. Tamko la Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe la kuitisha maandamano nchi nzima
kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba imesababisha Jeshi la Polisi
kumwita ili kutoa ufafanuzi wa kauli yake huku Bunge hilo likichepusha
mjadala na kutumia muda mrefu kujadili hotuba hiyo.
![]() |
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe |
Akizungumza jana na wajumbe wa Baraza Kuu la chama
hicho waliokuwa katika mkutano wa kuwachagua wajumbe wa Kamati Kuu,
katibu mkuu na manaibu wake, Mbowe alisema ameitwa na Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Isaya Mngulu, lakini
hatakwenda hadi atakapomaliza vikao vya Chadema.
“Jana (juzi) nilitoa kauli ya kufanya maandamano
nchi nzima, kauli hiyo imemfanya DCI kuniita...” alisema na kuongeza
kuwa msimamo wake na Ukawa uko palepale.”
Mapema jana, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa
Polisi, Paulo Chagonja alionya kuwa endapo Mbowe atafanya maandamano
kama alivyotangaza polisi hawatasita kumchukulia hatua za kisheria kwani
hiyo ni mara ya pili kutoa onyo dhidi yake.
“Ni wazi kwamba siasa zina mipaka yake na
zinapovuka na kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi
zinageuka kuwa jinai na wala siyo siasa tena,” alisema.
Juzi, katika Mkutano Mkuu wa Chadema, Mbowe alitoa
maazimio sita mazito ukiwamo utaratibu wa kuandamana nchi nzima kupinga
Bunge linaloendelea.
Bunge lahama mjadala
Mjadala wa Bunge jana, ulipoteza mwelekeo baada ya
wajumbe kadhaa waliopewa nafasi kuchangia, kuacha kujadili Katiba
badala yake ‘kurusha makombora mazito’ dhidi ya hotuba hiyo, kwa wana
Ukawa na Mbowe mwenyewe.
Baadhi ya wajumbe waliomzungumzia Mbowe na Ukawa
ni pamoja na John Komba, Amos Makalla, Fahmy Dovutwa, Dk Mary Nagu na
Mwenyekiti Samuel Sitta ambaye alikwenda mbali na kusema iwapo wajumbe
hao wa Ukawa walimpigia kura ili awabebe katika mambo aliyoyaita ya
kipuuzi, basi wasahau.
Kauli hiyo ya Sitta ilitokana na kauli ya Dovutwa
kueleza kile alichodai ni kiini cha Sitta kushambuliwa na wajumbe hao wa
Ukawa katika mikutano yao.
“Baada ya kuunda Ukawa, Mwenyekiti wa kikao
Freeman Mbowe akasema jamani mgombea wetu ni Samuel Sitta. Huyu atalinda
masilahi yetu. Tumekubaliana, lakini baadaye akasema yeyote
tutakayemwona anashirikiana na CCM tutamfanyizia,” alisema Dovutwa.
Hata hivyo, Mjumbe wa Bunge hilo, Vicent Mzena
aliomba mwongozo wa mwenyekiti akihoji inakuwaje Bunge hilo linajadili
mambo yaliyotokea nje ya Bunge badala ya kujikita kujadili utungaji wa
Katiba inayopendekezwa.
Akijibu mwongozo huo, Sitta alisema utayarishaji wa Katiba Mpya lazima mambo yote yanayohusiana na utungaji huo yasemwe bayana.
“Nashukuru sana Mheshimiwa Fahmy Dovutwa kwa
kutupa undani wa mambo kwa sababu kama hao watu walidhani kwa kunipigia
kura basi nitakubali upuuzi wowote basi kwa lugha ya siku hizi imekula
kwao,” alisema Sitta.
Makala ambaye ni Naibu Waziri wa Maji,
aliwafananisha Ukawa na kamati ya harusi inayogombania kupanga tarehe ya
sherehe badala ya kujikita kwenye kukusanya michango kutoka kwa
wajumbe.
“Nimpongeze Spika kwa kuweza kukaa na Ukawa kwa
sababu kuishi na hawa ni sawa na kubeba gunia la misumari kwa namna
wanavyodeka. Wamepotosha kila jambo tulifanyalo ili waonekane wana jipya
licha ya ukweli kwamba wanapigania katiba ya wachache. Tunaopigania
katiba ya wengi ni sisi tuliobaki.
“Nimesikia pale Profesa Lipumba (Mwenyekiti wa
CUF-Ibrahim) akisema kuna ufisadi mkubwa lakini yeye mbona alipokuwapo
hapa na alichukua posho? Kila tukikutana hapa anasema Makalla naona
mambo yanakwenda vizuri. Wao kutoka tu imekuwa ni nongwa.”
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbinga Mashariki,
John Komba alisema, “Jana Mbowe amekuwa amiri jeshi na tayari
ametangaza vita kwa kuandaa maandamano ya nchi nzima bila kibali cha
polisi hata kama jeshi hilo litalazimika kutumia risasi za moto. Huyu ni
mtu wa aina gani?
“Aliwasalimu wanachama wake kwa kusema ‘Ukawa…’ na
wao wakajibu ‘Tumaini letu…’ Naomba nitangaze personal interest
(masilahi binafsi) katika hili kwa sababu mimi ni Mkatoliki na
tunaposema hivyo huwa tunamaanisha imani ya hali ya juu. Kwa hili
nasubiri kauli ya maaskofu… wanapaswa kulikemea hili kwa nguvu.”
Komba amvaa Warioba
Komba aliendeleza mashambulizi yake kwa Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kumwita
mchochezi akisema amekuwa akiingilia mambo ya wajumbe kuwa wanakula
fedha za wananchi bila ya kukumbuka kuwa hata yeye (Warioba) alikula
fedha nyingi kuliko wabunge hao.
Chanzo Mwanachi
No comments:
Post a Comment