WANAFUNZI walemavu wa shule ya Msingi Kisosora mkoani hapa,
wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya mazingira ya shule hiyo iwe
rafiki kulingana na uhitaji wao ili waweze kufanya vizuri katika
mitihani yao.
Wanafunzi wenye ulemavu, Lucy Apolinali na Nyamkala Egness,
waliiambia Tanzania Daima kuwa, kilio chao kikubwa ni ukosefu wa vitabu
vya maandishi makubwa, miwani ya kusomea na usafiri.
"Tunakabiliwa na changamoto kubwa ya vitu hivi ambayo inatupelekea
kushindwa kufanya vizuri katika masomo yetu, ikiwa ni pamoja na
kushindwa kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea," alisema Nyamkala.
Awali, mwalimu wa walemavu shule ya Kisosora ambaye naye ni mlemavu, Selina Mremba, alisema shule yake inakabiliwa
na upungufu wa walimu wenye taaluma ya kufundisha makundi maalumu,
hali ambayo huathiri kiwango cha ufaulu wa wanafunzi walemavu.
Naye Ofisa Utetezi wa Haki za Walemavu Kituo cha Kutolea Mazoezi ya
Viungo kwa Walemavu (YDCP), Prisca Mwakasindile, aliwataka wanafunzi wasiwabague walemavu, badala yake washirikiane nao katika masomo,
stadi za kazi na michezo kwa lengo la kuwajengea elimu shirikishi ili
wanapomaliza shule wawe na cha kujivunia.
Shule ya Msingi Kisosora, ina wanafunzi walemavu 25 katika madarasa
tofauti, licha ya kukabiliwa na tatizo la upungufu wa vifaa,
miundombinu ya vyoo na majengo si rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu.
No comments:
Post a Comment