KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, ilirejea jana
jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza kambi ya wiki moja visiwani
Zanzibar, ambayo ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kujiandaa na msimu
ujao.
Ikiwa visiwani humo, Azam FC mbali na kujifua vilivyo pia ilipata
fursa ya kucheza mechi mbili za kirafiki, wa kwanza ikicheza na Kombaini
ya Wilaya Mjini na wa pili walikipiga na Taifa ya Jang’ombe, zote
ilishinda bao 1-0.
Unaweza kujiuliza ni kwanini ushindi kiduchu hivyo, kiukweli licha ya
washambuliaji kukosa nafasi nyingi za wazi lakini Kocha Mkuu Zeben
Hernandez, kwa sasa yupo kwenye kazi kubwa ya kukisuka kikosi kuingia
kwenye mfumo wake.
Kwa mujibu wa maelezo yake, jambo kubwa analolizingatia hivi sasa ni
kusuka eneo lake la ulinzi pamoja na kuifanya timu yake kwa nafasi
kupitia mfumo wake na kwa sasa mabao yanakuja kama ziada tu, lakini hayo
hayajamnyima nafasi ya kusema kuwa ana tatizo kubwa la ufungaji wa
mabao ndani ya kikosi chake.
Wakati kikosi cha Azam FC kikiwa mapumzikoni leo Jumatatu kikitarajia kurejea mazoezini kesho Jumanne asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika tovuti ya Azam na hapa unakuletea manufaa ya kambi hiyo kisiwani zanzibar
Matayarisho ya kisasa
Azam FC ikiwa Zanzibar ilivutia watu wengi na hii ni kutokana na
programu za matayarisho iliyokuwa ikitolewa na makocha wa kikosi hicho.
Kocha Mkuu Zeben na Msaidizi wake,Yeray Romero, Kocha Msaidizi wa
Viungo, Pablo Borges, wa Makipa Jose Garcia na Daktari Sergio Perez
Soto, waliwateka watu kutokana na kufanya programu tofauti tofauti za
mazoezi kila siku.
Makocha hao hawakuishia programu za uwanjani tu bali hata zile za nje
ya uwanja, ambazo baadhi yao ni zile za kufanya mazoezi makali
ufukweni, kufanya mazoezi ndani ya bwawa la kuogelea (swimming pool)
pamoja na ile mpya kabisa ya wachezaji kuendesha baiskeli barabarani,
ambayo hufanywa hata na timu kubwa barani Ulaya.
Mpaka sasa makocha hao wakiwa wamefikisha wiki tatu za mazoezi yao
wakiwa na lengo kubwa la kuifanya Azam FC kuwa timu ya kisasa ndani na
nje ya uwanja, tayari mwanga huo umeshaanza kuonekana kwa wachezaji
kutokana na programu za kisasa wanazopewa zinazoendana na vifaa vya
kisasa vya ufundishaji.
Mfumo wa uchezaji
Kama inavyojulikana ujio wa makocha hao kutoka Hispania ni kuifanya
Azam FC icheze soka la kuvutia pamoja na mafanikio Kitaifa na Kimataifa,
kwa muda mchache tu waliopo mpaka sasa timu imeonekana kubadilika
kwenye mfumo wa kiuchezaji.
Azam FC kwa siku za hivi karibuni kwenye mechi zake za majaribio,
imekuwa ikionekana kucheza soka la kueleweka tokea inapoanzisha mpira
hadi kufika kwenye eneo la hatari la timu pinzani huku wachezaji
wakicheza kwa nidhamu kubwa.
Lakini tatizo kubwa linalowakabili wachezaji wa Azam FC ni ugeni wa
mifumo mipya wanayopewa na makocha hao, jambo ambalo tayari Zeben
amelitolea ufafanuzi akisema itawachukua mwaka mzima wachezaji kuweza
kuushika ipasavyo mfumo wake wote.
Hivyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo tunaweza kuishuhudia
Azam FC mpya kabisa itakayokuwa ikitisha zaidi kila idara,
ikijitambulisha yenyewe kupitia soka safi inalocheza na litakaloipatia
matokeo bora uwanjani.
Ukabaji wa hali ya juu
Timu bora iliyokamilika haiangaliwi tu namna inayokuwa ikimiliki
mpira bali jicho jingine hutupiwa pale inapokuwa haina mpira, Je,
inawezaje kuurejesha mpira kwenye himaya yao pale inapopokonywa na
mpinzani?
Azam FC katika mechi zake za majaribio ilizocheza awali Azam Complex
na ikiwa kambini Zanzibar, imekuwa na uwezo mkubwa sana wa ukabaji pale
inapokuwa haina mpira, hii ikiwa ni sehemu ya mafundisho ya Zeben ambayo
amekuwa akiyafanyia kazi mara kwa mara mazoezini.
Mabingwa hao wanaodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi kabisa
cha Azam Cola, wachezaji wake wamekuwa na pumzi ya kutosha kwenye mechi
wanazocheza, huku wakianza kukaba kwa pamoja kutoka eneo la ushambuliaji
hadi ulinzi jambo ambalo limekuwa likiwapa shida sana timu pinzani
ilizocheza nazo mpaka sasa.
Inatisha kwa ufiti
Programu ya mazoezi makali ya viungo wanayoendelea kupewa wachezaji,
imefanikiwa kuwasaidia sana wachezaji mpaka sasa wakiwa wanaonekana na
nguvu kubwa.
Hata pale wanapogombea mpira na wachezaji wa timu pinzani nguvu hiyo
imekuwa ikionekana kwa wachezaji wa Azam FC kushinda mipira kirahisi
huku wakionekana wanafanya sana rafu kumbe hiyo inatokana na ufiti
waliokuwa nao.
Hivi sasa kila mchezaji amepewa programu yake ya mazoezi ya ‘gym’
kulingana na mwili wake ulivyo, ambayo hutakiwa kufanya kila siku kabla
ya mazoezi ya pamoja asubuhi.
Kubadilishwa namba
Moja ya vitu ambavyo bado makocha wa Azam FC wanavifanyia kazi ni
kuwajaribu wachezaji waliokuwa nao kikosini kucheza namba tofauti
tofauti uwanjani.
Wachezaji ambao mpaka sasa wameweza kuchezeshwa namna tofauti ni
Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, ambaye alitolewa kwenye eneo la
kiungo wa ukabaji alilolizoea hadi beki wa kati akicheza na Aggrey
Morris.
Baada ya Zeben kumaliza kumjaribu Himid katika nafasi hiyo, kwenye
kambi ya visiwani Zanzibar alihamia kwa kiungo mkabaji Jean Baptiste
Mugiraneza ‘Migi’, ambaye katika mechi zote mbili za huko alimchezesha
beki ya kati sambamba na Aggrey.
Migi aliyewahi kucheza nafasi hiyo kwenye mechi ya African Lyon msimu
uliopita, ameonekana kufanya vizuri sana katika kutekeleza majukumu ya
namba hiyo jambo ambalo limewafurahisha makocha.
Wachezaji wengine waliobadilishwa namba ni mabeki wa kati David
Mwantika na kinda Ismail Gambo, ambao kwa sasa wanachezeshwa kama mabeki
wa upande wa kulia.
Umakini kwenye usajili
Timu bora siku zote hujengwa na muunganiko wa wachezaji bora ili
kufikia mafanikio yaliyokusudiwa, wakati Azam FC ikiwa kwenye maandalizi
ya msimu mpya makocha wa timu hiyo wamefanikiwa kuwa makini kwenye
usajili.
Mpaka sasa zoezi la usajili likiwa linaendelea, wachezaji kadhaa
wamepata nafasi ya kufanya majaribio ya kujiunga na Azam FC, lakini
imekuwa ni ngumu kwa makocha hao kufanya uamuzi wa haraka wa kusema
mchezaji fulani asajiliwe.
Wachezaji ambao mpaka sasa wamemaliza wiki mbili na bado wanaendelea
kujaribiwa ni Fuadi Ndayisenga, Ibrahima Fofana, Bruce Kangwa huku Brian
Abbas akiwa ametimiza siku ya sita sasa tokea aanze majaribio.
Azam FC mpaka sasa imeshakamilisha usajili wa winga kutoka Medeama ya
Ghana, Enock Atta Agyei (18), ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili
wiki iliyopita na ameshatua nchini tokea Jumamosi iliyopita tayari
kabisa kuanza mazoezi.
Kila kitu umoja
Namna pekee ya timu yoyote kufikia mafanikio yaliyokusudiwa si tu
kuishia kwenye kusajili wachezaji bora na kuchukua makocha bora, bali
suala la kutengezeza mshikamano na umoja ndani ya timu nalo ni moja ya
jambo kubwa sana la kufanikisha hilo.
Ukiingalia Azam FC hivi sasa imebadilika sana hasa linapokuja suala
la umoja, makocha wapya wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha umoja
ndani ya timu, ambapo kila kitu wachezaji hufanya kwa umoja bila
kutengana.
Ni jambo la kufurahisha sasa hivi ukiona namna wachezaji wa Azam FC
wanaposhangilia mabao yao kwenye mechi hizi za majaribio, kwani wamekuwa
wakipongezana kwa pamoja wakia na furaha ya pamoja kila wanapofunga.
Hakuna masikhara
Moja ya mambo makubwa ambayo makocha wapya wamefanikiwa kudhibiti, ni
kujenga nidhamu kubwa kwa wachezaji ndani na nje ya uwanja.
Makocha hao wamekuwa wakisisitiza nidhamu kwa wachezaji pale
linapokuja suala la kazi iliyowafanya wawe Azam FC na hakuna muda wa
masikhara, na ili kulidhibiti suala hilo wamefanikiwa kuweka sheria
mbalimbali kwa wale watakaoshindwa kwenda kinyume na hilo.
CHANZO AZAM TOVUTI
No comments:
Post a Comment