WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amevitaka viwanda vya sukari nchini kuongeza mikakati ya uzalishaji
zaidi ili mwaka 2020 Tanzania iwe imefikia kiwango cha kuzalisha
asilimia 100 ya mahitaji yake.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumanne, Agosti 02, 2016) wakati alipotembelea kiwanda cha sukari cha
Mtibwa kilichoko mkoani Morogoro ambapo amesisitiza viwanda vya ndani
vizalishe zaidi ili kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya
nchi.
Amesema Serikali imejikita katika
kuimarisha na kulinda viwanda vya ndani nchini hivyo ni vema viwanda vya
sukari vikaweka mikakati ya kuzalisha kwa wingi ili kuondokana na
uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje.
“Kiwango cha mahitaji ya sukari
nchini ni zaidi ya tani 400,000, nimeiagiza Bodi ya Sukari kukaa na
wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kufanya utafiti ili
tujue mahitaji halisi ya sukari,” alisema.
Waziri Mkuu amesema Serikali
imeweka mkakati wa kulinda viwanda vya ndani kwa kuziongezea kodi bidhaa
zinazotoka nje ambazo zinazalishwa na viwanda vya ndani ikiwemo sukari
hivyo wenye viwanda hawana budi kuzalisha kwa wingi zaidi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka
wamiliki wa viwanda vya sukari nchini kutoa motisha kwa wakulima wa nje
kwa kununua miwa yao kwa bei nzuri na kuwalipa kwa wakati ili nao
wanufaike na uwepo wa viwanda hivyo na kuwa walinzi wa uwekezaji huo.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano
Mwandamizi wa kiwanda hicho, Ibrahim Juma amesema kwa sasa kiwanda
kinazalisha tani 20,000 kwa mwaka na wanatarajia kuongeza uzalishaji
hadi kufikia tani 70,000 ifikapo mwaka 2021.
Juma alisema uzalishaji wa sukari
kiwandani hapo ulipungua kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje
hivyo aliipongeza serikali kwa kudhibiti uingizwaji holela wa sukari
kutoka nje jambo litakalosaidia ukuzaji wa viwanda vya ndani.
Meneja huyo alisema kuwa kwa sasa
wameanza upanuzi wa mashamba kiwandani hapo ambapo wanatarajia kuongeza
hekta 400,000 lengo likiwa ni kutimiza ndoto ya Serikali ya kuifanya
Tanzania ijitosheleze katika uzalishaji wa sukari.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 02, 2016.
No comments:
Post a Comment